Wednesday 1 June 2016

KENYA HAINA UHURU ISIPOKUWA RAIS

Taifa la Kenya kwa miaka hamsini na tatu sasa limejivunia Uhuru.
Tangu mbeberu kuondoka nchini humu na kuacha mababu zetu wajitawale wenyewe, Kenya imepiga hatua si haba. Si katika elimu, kilimo, afya, usalama, nitaje tu japo machache, almuradi nchi imepiga hatua.
Lakini tutazame jambo hili kwa undani zaidi. Je, nchi hii imepiga hatua za kusonga mbele ama kurudi nyuma. Ninapotazama kwa karibu sana naona kuwa Kenya imepiga hatua za kinyumenyume.
Nchi hii imegeuka jongoo ambaye ukimfungia njia ya kwenda mbele, ataanza kurudi kinyumenyume na kukupa taswira kuwa bado yuko sawa huku ukishindwa kubaini kichwa chake ki wapi. Kwa vyovyote vile, bado yuasonga tu.
Viongozi wa Kenya kwenye dhifa ya chakula cha mchana Ikulu ya Nairobi
Kwa wanaonijua kwa karibu, mimi ni mzalendo imara. Lakini ifikapo kwa kusema ukweli, watu wengi ambao ni wazalendo huonekana kama watu wasioipenda nchi yao.
Kwa wale ndugu Wakristo kama mimi, Biblia yatueleza wazi katika kitabu cha Yohana Mtakatifu mlango wa nane, msitari wa thelathini na mbili kuwa;
"Mtaujua ukweli na ukweli huo utawaweka huru"
Kwa hivyo ifikapo kwa maswala ya kusema ukweli, acha niseme japo kwa kiduchu.
Miaka hamsini na tatu iliyopita, mkoloni alifunganya na kurudi Uingereza. Au kwa lazima ama hiari, almuradi alituachia nchi yetu.
Mababu zetu kwa wakati huo walikuwa na utaifa wa kutajika kwa kuwa walikuwa wamepitia shida tumbi nzima chini ya mkoloni. Walijua ni nini maana ya undugu.
Viongozi waliotangulia nchini humu walikuwa wamesomea vilivyo ujuzi wa kuwaua watu kutoka kwa mkoloni.
Kila aliyeonekana 'tisho' kwa serikali alitolewa uhai. Iwe kwenye ajali, kuliwa na wanyama pori, kupotea na maiti yake kupatikana porini…
Kila aliyeingia mamlakani na kuonja 'utamu' (iwapo mamlaka yana utamu wowote) wake alikatalia mamlakani na kupelekea wananchi kughadhabika.
Wizi wa kura zimefanywa mbele ya kila mkenya.
Miaka ishirini na nane iliyopita, tarehe ishirini na moja mwezi Machi mwaka elfu moja kenda mia themanini na nane, nchi hii ilishiriki uchaguzi wa 'Mlolongo' chini ya aliyekuwa rais wa wakati huo Daniel Moi.
Uchaguzi huo umezungumziwa hadi leo kuwa ulikuwa Huru na wa Haki (kumbuka kisa cha jongoo awali). Huo ndio ulikuwa utaifa. Huo ndio ulikuwa umoja. Huo sio uzalendo ninaouzungumzia kwenye nakala hii.
Uchumi wa taifa hili umedorora kwa kiwango cha kutajika. Hivi majuzi, Uchumi wa taifa la Tanzania umetajwa kama nambari wani katika eneo la Afrika ya Mashariki; Miezi kadhaa baada ya Pombe Magufuli kuchukua hatamu za uongozi nchini humo.
Kenya; nchi iliyojulikana ulimwengu mzima kwa muda mrefu  kama kitovu cha usalama ikarudi na kuwa eneo la kukuza ugaidi na magaidi.
Mwaka elfu mbili na kumi, wakenya kwa pamoja waliipigia kura katiba mpya. Katiba ambayo inahujumiwa na kukiukwa kila uchao.
Hadi kufikia sasa, kuna wakenya waliopigania uhuru, wakateswa na wengine kuawa lakini kufikia sasa bado wao na familia zao hawajafidiwa.
Umaskini ambao umekithiri nchini huenda ukatolewa tu kwa maombi. (Kwani hatuna viongozi ambao hufanya mikutano ya maombi)?. Ikiwa mikakati itawekwa na viongozi kupiga vita umaskini, basi haitachukua muda wa chini ya miaka hamsini na tatu tena ili mpango huo ufue dafu.
Hii ni kwa sababu ufisadi ambao ndio wimbo wa kila siku humu nchini utalemaza shughuli hiyo, huku kila mmoja kwenye ofisi za serikali akitaka kuvuna asipopanda.
Nikiandika kupita hapo, huenda nikapatwa na kichefuchefu, nikohoe na kutapika uzalendo wangu.
Iwapo huu ndio uhuru waliopigania wazee wetu, basi sina budi kusema kuwa Kando na rais UHURU, Kenya haina Uhuru mwingine.


Ee Mungu Nguvu Yetu,
Ilete Baraka kwetu,
Haki iwe ngao na mlinzi,
Na tukae na Undugu,
Amani na UHURU,
Raha tupate na ustawi.

Na Kisabuli Caleb.

Thursday 26 May 2016

USICHOKIJUA KUHUSIANA NA ALIYEKUWA WAZIRI WA NYUMBA MAREHEMU SOITA SHITANDA

Kifo cha aliyekuwa mbunge wa Malava Soita Shitanda kimewaacha wengi na huzuni, huku viongozi wengi wakijitokeza na kutuma risala zao za rambirambi kwa familia, wakazi wa eneo bunge la Malava na wakenya wote kwa jumla kwa kumpoteza kiongozi huyo.

Wengi wamemtaja kama kiongozi shupavu ambaye alifanya kazi yake bila ubaguzi, na kwa uhodari wa kutajika.

Ungependa kujua ni kwa nini kiongozi huyo amemiminiwa sifa riboribo? Safiri nami nikujulishe.

Aliyekuwa mbunge wa Malava, Marehemu  Peter Soita Shitanda
Marehemu Shitanda alizaliwa tarehe tisa mwezi Novemba mwaka wa elfu moja kenda mia hamsini na tisa katika kijiji cha Kabras, Malava na kupashwa tohara mwaka wa elfu moja kenda mia sabini na mbili.
Alijiunga na shule ya msingi ya Tande huko Malava mwaka wa elfu moja mia tisa sitini na saba kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Malava kwa kiwango cha O-Level alikosomea hadi mwaka wa elfu moja mia kenda sabini na saba.
Mwaka mmoja baadaye, Shitanda alijiunga na chuo cha ufundi cha Kenya na baadaye kufanya kazi kama mwanafunzi wa uhasibu kwenye afisi za mwanasheria mkuu.

Mwaka wa elfu moja mia tisa themanini na tatu, akajiunga na chuo cha Strathmore alikokuwa kwa miaka miwili na punde baada ya kutoka chuo, akafanya kazi katika vitengo tofauti vya uhasibu katika wizara ya fedha nchini Kenya.

Mnamo mwaka wa tisini na saba, Shitanda aliiacha kazi ya uhasibu na kuingilia siasa. Aliwania kiti cha ubunge katika eneo bunge la Malava na kumshinda aliyekuwa kwa wakati huo waziri wa afya na mbunge wa eneo hilo Joshua Angatia katika tiketi ya chama cha Ford Kenya, chama kilichokuwa na umaarufu sana katika eneo la magharibi.

Mnamo mwaka wa elfu mbili na mbili Shitanda aliwania tena kiti hicho na kushinda na kufanywa naibu waziri katika afisi ya rais Mstaafu Mwai Kibaki. Miaka mitatu baadaye, Shitanda aliteuliwa kama waziri wa nyumba.

Kwenye uchaguzi wa mwaka wa elfu mbili na saba, Shitanda aliwania na kushinda tena kiti cha ubunge cha Malava na kumfanya kuwa mbunge ambaye amewahi kuongoza eneo hilo kwa muda mrefu Zaidi tangu taifa la Kenya kunyakua Uhuru. Aliteuliwa tena waziri katika wizara ya nyumba mwaka uo huo.

Aidha, Shitanda aliwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Kakamega mwaka wa elfu mbili na kumi na tatu na kushindwa na Gavana wa sasa wa Kaunti hiyo Wycliffe Oparanya.

Kulingana na ripoti, kiongozi huyo amekuwa akiugua ugonjwa wa kisukari kwa miaka miwili hadi alipokumbana na mauti Jumanne tarehe ishirini na nne mwezi Mei mwaka huu.

Shitanda alifariki siku tatu tu baada ya kakake mkubwa Walucho Shitanda kuzikwa siku ya Jumamosi, tarehe ishirini na moja Mwezi Mei mwaka huu.
Kando na Walucho, marehemu Shitanda ana kaka wawili; Ngaira na Mwombe na dada watatu, wote wako hai. Amewaacha watoto wanne.

Rais Uhuru Kenyatta amemtaja kiongozi huyo kama aliyeipenda nchi na aliyejitolea katika kufanya kazi yake.

Yote tisa, Kumi? Mungu ailaze roho yake mahali pema.


Na Caleb Kisabuli