Tuesday 20 October 2015

HAKUNA CHA KUSHEREHEKEA SIKU YA MASHUJAA

Mimi ni Mkenya mzalendo, mpenda amani. Lakini leo niruhusu nifungue roho yangu, ninene kwa ufupi.

Tunasherehekea siku ya Mashujaa, tarehe ishirini ya mwezi wa kumi kila mwaka nchini Kenya. Swali ninalouliza ni je, kuna lolote la kusherehekea?

Kama hekaya za abunuwasi zingekuwa matendo, basi taifa hili lingekuwa miongoni ma mataifa bora ulimwenguni.

Ni taifa ambalo wananchi walio kwenye mitandao ya kijamii kama vile Twitter, almaarufu Kenyans on Twitter (KOT) wana busara kuliko maafisa wa serikali.

Taifa lililojaa ubinafsi, wizi, uporaji wa mali ya umma na uroho.

Mwandishi mmoja akasema ni taifa la matajiri kumi na maskini milioni kumi. Yaani kwa kila mlalahai mmoja tuna walalahoi milioni moja.

Hamna umuhimu katika kuisherehekea siku hii, ambayo pia imebinafsishwa kwa minajili ya wachache wanaothamini tumbo zao kuliko mishahara ya wanaotoa huduma kwa wale wakenya maskini kama vile walimu.

Kama vile vyama vya kisiasa vilivyo na wafuasi, vivyo hivyo ndivyo ilivyo na maafisa wakuu katika serikali na wanaowafuata ni ndugu, jamaa na marafiki, tena sio wote, wale wa karibu.

Nchi ambayo imewatafuna, kuwala na kuwameza mashujaa wao. Kila aliyepigania haki hayupo tena, kwa kuwa watu fulani hawakuwaruhusu kuishi kuona matunda ya waliyokuwa wakipigania.

Ukweli mchungu ni kwamba, hata wangefufuka waliokufa katika kupigania uhuru - ambao hadi sasa hatujauona - bila shaka wangeanguka na kufa mara tena kutokana na mshtuko wa moyo.

Serikali za hapo awali ziliwatesa na kuwaua watu waliotaka kulikomboa taifa hili.

Yeyote aliyekataa kumbeba jogoo wake mkobani na kuwika kila asubuhi, basi alikuwa mashakani na kila aliyetaka kuwa salama, basi angeimba wimbo sawa na wa mwenye jogoo.

Jogoo angeishi miaka mia moja. Ameishi miaka hamsini na miwili sasa, safari bado ndefu kwa kuwa wenye kujua hesabu wataona wazi kuwa ana miaka mingine arubaini na nane.

Sitazungumza sana kuhusiana na historia ya mashujaa na matatizo wanayoyapitia wakenya kwa sasa, kwa kuwa sote twayafahamu vyema mambo haya.

Usifadi ndio wimbo katika kinywa cha kila Mkenya.

Mali ya Umma inachukuliwa na mababe wa uongozi. Ardhi nayo sitasema inanyakuliwa. Vijana nchini hawana kazi, hilo sitataja. Umaskini umekithiri, sisemi. Usalama haupo, hujui hilo pia?

Ufujaji wa pesa za umma ndiyo shughuli ya magavana. Pazia, Kitandazi, Lango, Rukwama, kuwahamisha watoto wanaorandaranda mitaani hadi kwenye 'Kaunti zao', nitaje tu machache.

Kazi waliyofanya mashujaa; waliouawa kikatili, yote ni bure kwa kuwa uhuru bado hatujaupata. Ukoloni mambo leo umekithiri. Walio na mali wanaongezewa. Wasio na mali hata kile kidogo walicho nacho wamenyang'anywa.

Yote tisa, kumi? Lililo na mwanzo halikosi mwisho. Nina imani na matarajio kuwa maovu haya yatakoma siku moja.

Caleb Kisabuli

No comments:

Post a Comment