Wednesday 16 March 2016

Je, IEBC ifutiliwe mbali?

Chaguzi ndogo za hivi karibuni katika kaunti ya Kericho na eneo bunge la malindi zimeonyesha kuwa Tume ya Uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC haiaminiwi na wakenya.

Wanasiasa kutoka mirengo tofauti wamelalamikia chaguzi hizo mbili wakisema hazikuwa huru na za haki.

Swali langu ni je, Ni nani anayesema Ukweli?

Ni Jubilee, au KANU? Ni CORD au wapinzani wao?

Kwa mfano, kiongozi wa walio wengi kwenye bunge la kitaifa Aden Duale amesema kuwa uchaguzi wa malindi haukuwa wa haki kwa manufaa ya muungano pinzani CORD.

Huku hayo yakijiri, katibu mkuu na Mwenyekiti wa chama cha KANU Nick Salat na Seneta Gideon Moi mtawalia wamesema kuwa uchaguzi wa Seneta wa kaunti ya Kericho pia haukuwa wa haki kwa manufaa ya Naibu Rais William Ruto na mrengo wa Jubilee kwa jumla.

Swali langu ni je, ikiwa madai haya yangepatikana na ukweli, basi IEBC inamfanyia nani kazi?

Wanasiasa wetu wamesababisha wananchi kukosa imani na tume hii kutokana na matamshi yao kinzani ambayo kwa mtazamo wangu yanaletwa na sababu za kibinafsi, uroho na uchoyo.

Kama IEBC itarudia makosa ya ECK yaliyotokea mwaka wa elfu mbili na saba, basi haina haja ya tumee hii kubaki ilivyo.

Ama ifanyiwe mabadiliko kwenye uongozi wake au ifutiliwe mbali ili tume nyingine itakayoaminiwa na wananchi wa Kenya itengenezwe.
Ikiwa tume hii ya IEBC imekosa kuwahamasisha wakenya kikamilifu kuhusiana na kuandikisha wapiga kura, basi sioni ikiwa iko kwenye nafasi bora ya kuusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Hata hivyo, hizi ni kelele za kisiasa na mara nyingi huwa na propaganda nyingi na uongo usiopimika. Pengine twaweza kuipa tume hii muda zaidi wa kufanya kazi.

Na C Okay

No comments:

Post a Comment